• Ndugu Mgeni Rasmi, Joseph Kashushura Rwiza, Mkurugenzi Mtendaji, Kasulu Vijijini
• Mwakilishi wa MkurugenziMKuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote
• Mrajisi Msaidizi, Mkoa wa Kigoma
• Mwasisi wa Wazo la Mtandao Jamii na Mkurugenzi Mkuu, Tanzania Community Networks Alliance, Dr. Jabhera Matogoro
• Wakurugenzi na wafanyakazi wote wa Tanzania Community Networks Alliance
• Wenyeviti wa Mitandao Jamii Mliopo kutokea, Kondoa, Nyasa, Tarime na Wenyeji, Kasulu
• Mwakilishi wa KICTANet, Catherine Kyalo
• Mwakilishi wa Omuka Hub, Dorice Kaijage
• Wawezeshaji wa mada mbali mbali
• Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa,
• Wadau wa Maendeleo na Asasi za Kiraia;
• Ndugu Wageni Waalikwa, Waandishi wa habari na wadau wote wa mawasiliano;
• Mabibi na Mabwana;
Nawasalimu kwa Jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Bwana Yesu asifiwe!
Asalaam Alaykum
Habari za Asubuhi
Ndugu Mgeni Rasimi, nitumie fursa hii kumshukuru MUNGU mwingi wa rehema kwa kutujalia kufika hapa tukiwa wazima waafya tele. Miongoni mwetu wamo watu zaidi ya 20 ambao wamesafiri kutoka nje ya Wilaya ya Kasulu, na nje ya Tanzania, tunamshukuru Mungu kwa kutufikisha hapa salama.
Pili, tunapenda kukushukuru wewe Ndugu Mgeni rasmi kwa kukubali kwako kuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa kongamano hili na pia tuna kukaribisha sana ushiriki pamoja nasi katika siku hii muhimu na usikilize historia fupi, malengo, mafanikio na changamoto mbalimbali tunazopata katika uendeshaji wa program yetu ya Huduma za Mawasiliano ya Kijamii kwa wale ambao hawajafikiwa na hasa namna ambavyo tumejipanga kuondoa pengo la matumizi ya mtandao yaani usage gap.
Tatu, Ndugu Mgeni Rasmi, tuna washukuru wageni wetu pamoja na wenyeji kwa kutenga muda wao na kutumia raslimali zao kuhudhuria katika kongamano hili la tatu ambalo linalofanyika hapa Kasulu ndani ya Viunga vya Kasulu Motel.
Ndugu Mgeni Rasmi, ndugu viongozi na Wadau wa Sekta ya Mawasiliano, Kongamano hili huwa linafanyika mara moja kwa mwaka nchini Tanzania toka lililopoanzishwa Mwaka 2020. Kongamano la kwanza lilifanyika Mwaka 2020 kule Kondoa, na la pili lilifanyika Mwak 2021 katika Jiji la Dodoma. Tunafurahi kuona kongamano la Tatu likifanyika ndani ya Mkoa wa Kigoma, Wilaya ya Kasulu Mwaka huu wa 2022. Lengo kuu la mpango huu wa Huduma kwa Jamii ni kuunganisha waliotengwa (Connecting the Unconnected) katika huduma za matumizi ya mtandao kupitia Teknolojia mbali mbali ikiwemo ile ya mawimbi ya TV. Tunalenga kuzifikia taasisi zote za Tanzania ifikapo 2025 ambazo ni pamoja na baadhi ya shule za msingi, sekondari, vyuo vya kati, vyuo vikuu na ofisi zote za Serikali.
Ndugu Mageni rasmi, mafanikio ambayo kwa hapa Tanzania toka kuanzishwa kwa program hii yamefanikiwa ni kufunga mitambo ya mawasiliano kupitia mawimbi ya TV katika mji wa Kondoa ambayo inahudumia utoaji wa mtandao katika taasisi tatu za Serikali ambazo ni Shule ya Wasichana Kondoa, Chuo cha Ualimu Bustani na Shule ya Sekondari Ula na pia kushirikiana na wadau mbali mbali tumeweza kutoa huduma za TEHAMA katika Mashule kwa kushirikiana na African Child Project katika Mkoa wa Songea, Mara na Kigoma.
Ndugu Mgeni Rasmi, Kituo cha Jamii cha TEHAMA ambacho umekifungua leo kilikuwa na malengo ya kuwa na Kompyuta kumi kwa kuanzia hivyo tuna upungufu wa kompyuta sita na tunakuomba Mgeni Rasmi ili uendelee kutushika Mkono. Changamoto nyingine kwa sasa katika nchi yetu ya Tanzania ni pamoja na vibali vya muda mfupi vinavyotolewa na mamlaka ya mawasiliano TCRA nchi Tanzania hasa kwenye Television White Space na Community Network. Ndugu Mgeni Rasmi, changamoto nyingine ni kukosekana na sera za kudumu zinazotambua Mawasiliano ya jamii kupitia mawimbi ya TV na Community Network.
Ndugu Mgeni Rasmi, tunaleta kwako maombi maalumu ambayo yatatusaidia kuondoka katika kizingiti hiki ambacho tumegota kwa kupendekeza yafuatayo;
Mosi, kuiomba mamlaka ya mawasiliano Tanzania TCRA kutoa vibali vya muda mrefu au vya kudumu kwa wadau wanao anzisha miradi kama hii ya maendeleo ya mawasiliano,
Pili, kuiomba Wizara ya Habari, Mawasiliano ya Habari na Teknolojia ya Habari kutengeneza sera madhubuti zinazotambua mawasiliano ya jamii kupitia mawimbi TV na community network nchini Tanzania.
Tatu, tunaiomba ofisi yako kupitia idara ya maendeleo ya jamii kuendelea kushirikiana nasi kutoa mafunzo kwa makundi mbali mbali yenye lengo la kupunguza pengo la matumizi ya Mtandao yaani to address usage gap in Tanzania.
Ndugu mgeni rasmi, naomba kuhitimisha kwa kuwashukuru wale wote ambao kwa namna moja ama nyingine wamefanikisha kongamano hili kubwa. Kongamano hili limefadhiriwa na Association for Progressive Communication (APC) lenye Makao Makuu yake kule Africa Kusini, AFRINIC lenye Makao Makuu yake kule Mauritius, na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote lenye Makao Makuu yake Jijini Dodoma. Hata hivyo Mheshimiwa Mgeni Rasmi, tunatambua wale wote ambao waliotoa raslimali zao (muda na fedha) katika kufanikisha kongamano hili. Ndugu mgeni rasmi, kauli mbiu ya kongamano hili isemayo “Ujuzi wa Kidigitali Katika Kupunguza Pengo la Matumizi ya Mtandao” Yaan, “Digital Literacy toward Addressing Usage Gape in Tanzania” tunaamini kuwa mtandao jamii ulio bora, ukiimarishwa unaweza kutupeleka kwa kasi katika maendeleo ya watu ambayo ndiyo nia kuu ya serikali ya awamu ya sita.
Mheshimiwa Mgeni Rasmi, kituo ambacho umekizindua leo ni kituo cha kwanza kumilikiwa na Mtandao Jamii kwa lengo la kutoa mafunzo na huduma mbali mbali zenye lengo la kupunguza pengo la matumizi ya Internet.
Mhe. Mgeni rasmi, baada ya kusema hayo sasa napenda kukukaribisha rasmi katika ufunguzi wa Kongamano hili la Tatu la Wadau wa Masuala ya Mtandao Jamii Nchini.
MUNGU IBARIKI AFRIKA
MUNGU IBARIKI TANZANIA
Asanteni kwa Kunisikiliza.